DKT.ABBASI,BALOZI ANISA WAJADILI MIKAKATI KUITANGAZA TANZANIA INDIA


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbasi leo amekutana na kufanya magungumzo na Balozi wa Tanzania nchini India, Balozi Anisa Mbega juu ya mikakati zaidi ya kuutangaza utalii wa Tanzania. 

“Tangu Mhe. Rais alipofanya Filamu ya Tanzania The Royal Tour pamoja na juhudi za sekta binafsi lakini na nyie Mabalozi nchi yetu imeendelea kupokea mafuriko ya watalii. Lakini bado tunahitaji kuongeza mikakati zaidi hasa kwa nchi kama India yenye watu takribani Bilioni 1.4 bado ni soko kubwa tunalotakiwa kulifikia kimkakati zaidi,” alisema Dkt. Abbasi ambaye yupo jijini Delhi kuhudhuria pia Mkutano wa Kamati ya Urithi wa Dunia ya Unesco.

Alitoa mfano jinsi mikakati hiyo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan na wadau wenfine ilivyosaidia kupandisha mapato ya sekta ya utalii kwa ujumla

kutoka Dola Bilioni 1.3 tu mwaka 2021 kabla ya Royal Tour na sasa yamepanda hadi kufikia Dola Bilioni 3.57 Mei mwaka huu na kuifanya sekta ya utalii kuongoza nchini kwa kuleta fedha za kigeni ikifuatiwa na madini (Dola Bilioni 3.1) na uchukuzi (Dola Bilioni 2.5). 

Kwa upande wake Balozi Anisa alisema India ni soko kubwa na hivyo Ubalozi pamoja na mikakati mbalimbali wanayoendelea nayo ikiwemo makongamano ya utalii katika miji ya India amefurahishwa na ujio wa Katibu Mkuu wa sekta hiyo kwani utaimarisha mikakati waliyoanza kuitekeleza.

Post a Comment

Previous Post Next Post