KINANA ATAJA SIFA ZINAZOMFANYA MZEE MALECELA AENDELEE KUHESHIMIKA


MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulurhaman Kinana, amemwelezea Waziri Mkuu Mstaafu John Malecela kuwa mmoja wa viongozi waliopata mafanikio makubwa katika uongozi nchini, Afrika Mashiriki na duniani kwa ujumla.

Kinana ameeleza hayo leo Aprili  21, 2024 jijini Dodoma katika hafla ya kumbukizi ya kuzaliwa Mzee Malecela iliyofanyika nyumbani kwake Mtaa  wa kilimani jijini humo.Mzee Malecela amesherehekea kutimiza umri wa miaka 90

"Watu waliopata bahati ya kulelewa na mzee Malecela katika uongozi ni pamoja na mimi.Mzee Malecela ana uzalendo mkubwa na serikali hii.
 
"Ni mzee mwenye busara, kwa kauli ya haraka ukimuacha Baba wa Taifa (Hayati Mwalimu Julius Nyerere), Ali Hassan Mwinyi (Hayati Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili), kiongozi pekee aliyepata nafasi ya kuhudumia Afrika Mashariki, Afrika na duniani Hadi kuwa mtu mashuhuri duniani ni Mzee Malecela."

Kinana amesema moja ya sifa ya Malecela anajua kupima ni wakati gani wa kuchukua hatua gani,  na wakati gani wa kufanya maamuzi, ndio maana ameendelea kuheshimika.

"Mzee Malecela Chama Cha Mapinduzi (CCM)  kinatambua mchango wako katika kukijenga Chama hiki. Nakupongeza kwa kutimiza miaka 90, Mwenyezi Mungu tunamuomba akupe umri wa ziada," amesema.

Post a Comment

Previous Post Next Post