KUZUIA USAFIRISHAJI WA MADINI GHAFI NJE KULETA FURSA ZA AJIRA NCHINI


Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) kimechukua hatua muhimu kulingana na Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na marekebisho yake ya 2017 ambayo inalenga kuzuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi. 

Kupitia ziara iliyofanyika leo, Machi 21, 2024, Kaimu Mratibu wa Kituo hicho, Ally Maganga, ameeleza juhudi za TGC katika kuimarisha Sekta ya Madini kwa kuongeza thamani ya madini nchini.

Maganga ameeleza kuwa TGC imejikita katika kutoa mafunzo ya kuongeza thamani ya madini, akisisitiza faida kubwa za madini yaliyoongezwa thamani ikilinganishwa na madini ghafi. Kupitia sheria hii, lengo ni kuhamasisha uanzishaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya madini ili kuleta fursa zaidi za ajira na mapato ya kigeni nchini.

Akifafanua zaidi, Maganga amesisitiza kwamba sheria inawazuia kusafirisha madini ghafi nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa fursa za ajira zinapatikana ndani ya nchi. Aidha, TGC inapanga kupeleka vijana kupata uzoefu na utaalam katika nchi zenye ushirikiano, kama vile Thailand, ili kuongeza idadi ya wataalam wenye manufaa kwa Taifa.

Kuhusu mikakati ya TGC, Maganga ameeleza kuwa wanapanga ujenzi wa jengo la kisasa lenye ghorofa nane, upanuzi wa huduma za maabara, kuanzisha makumbusho ya madini ya vito, na kufanya utafiti wa masuala ya madini ya vito nchini. Haya yote yanakusudiwa kuwa chachu ya mageuzi katika Sekta ya Madini, hususan katika uongezaji wa thamani ya madini ya vito.

Post a Comment

Previous Post Next Post