KAMATI YA LAAC YARIDHISHWA NA MRADI WA JENGO LA UTAWALA HALMASHURI YA WILAYA YA MOSHI


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC)  imeridhishwa na usimamizi wa mradi wa ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Moshi.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Ester Bulaya (Mb) amesema, kila mtendaji akiwajibika hakutakuwa na shida ya kufuatiliana kwa kuwa  lengo la Kamati ya LAAC ni kutengeneza nidhamu ya fedha za Serikali.

“Tutamfuata mtu mmoja mmoja alipo sababu kuna  wengine wanaweza kuzembea wakiamini mzigo wa uzembe ataubeba Mkurugenzi Kamati hii imesema  kila mtu atabeba mzigo wake ikiwa pamoja na wakuu wa Idara ili kutengeneza uwajibikaji katika Halmasahuri zetu” amesisitiza Mhe. Bulaya

Mhe. Bulaya ametoa wito kwa watendaji hao kuendelea kusimamia miradi vizuri kwa uadilifu na usimamizi  mzuri na kuwaeleza  hakuna watu wengine wanaoweza kuiendeleza nchi yao zaidi ya watanzania wenyenye hivyo, ni vizuri kuwa wazalendo na  wafuatiliaji katika kujiletea maendeleo.

Kwa upande wa Mhe. Michael Mwakamo (Mb) akisoma mapendekezo kwa niaba ya Kamati hiyo amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kukamilisha mradi wa kituo cha Afya Uru  kama yalivyobainishwa kwenye taarifa ya CAG ikiwa pamoja na ufungaji wa vitanda 18, ununuzi wa taa maalumu kwa ajili ya chumba cha upasuaji pamoja na  kuhakikisha umeme unaingizwa.

Amemtaka Mkurugenzi kuwasilisha mchanganuo maalumu wa fedha zote zilizotumika katika  kituo hicho  kabla ya tarehe 30 Machi, 2024.

Vile vile Kamati imeitaka Ofisi ya Rais -TAMISEMI kufanya tathmini na kujiridhisha juu ya maombi ya fedha  Halmashauri  walizoziomba kiasi cha sh. 101,035,420.63 kilichobakia kwenye ujenzi wa Jengo la Halmashauri.

Awali taarifa iliyosomwa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Jengo la Halmashauri  imeeleza kuwa manufaa ya mradi ukikamilika utasaidia  kuendeleza shughuli za  utumishi na uboreshaji wa huduma za wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi wapatao 535,803  katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutumishi.

Aidha, katika taarifa hiyo pia imeeleza pamoja na mradi huo kukamilika lakini kuna kiasi cha sh. 101,035,420.63 kimebakia ambazo wataomba kibali TAMISEMI kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ambayo haikuwepo kwenye mpango kama ujenzi wa mgahawa wa watumishi, ujenzi wa ofisi ya madereva, ujenzi wa choo cha nje, ununuzi wa samani za wakuu wa idara na vitengo  na  ujenzi wa vibanda vya huduma za fedha.

Katika hatua nyingine   Kamati imeitaka Halmashauri hiyo  kuwa na taarifa kamili katika matumizi ya fedha za  ujenzi wa kituo cha Afya cha Uru na kusema  Kamati haijaridhishwa na matumizi ya fedha  zaidi ya sh. milioni 500 kutumika ikiwa vituo hivyo vinajengwa kwa sh. milioni 500 .

Aidha, katika Halmashauri ya Wilaya ya Moshi Kamati ilikagua Jengo la Halmashauri, Kituo cha Afya Uru na Shule ya Sekondari Njia panda.

Post a Comment

Previous Post Next Post