Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Tisha Mama Foundation Mhe. Mahawanga Janeth, amezindua Program ya Sanaa ya Uchoraji kwa Mabinti na Vijana katika Kituo cha Don Bosco, Upanga Mkoani Dar es Salaam.
Katika Uzinduzi huo Viongozi mbalimbali walihudhuria wakiwemo Wah. Madiwani wa Viti Maalumu kutukoka Halmashauri ya Wilaya ya Kinondoni, Diwani kata ya Mbezi Juu, Meneja wa Miradi wa CRDB Bank Ndg. Baraka Kiyalo, Viongozi wa
Serikali za Wanafunzi wa Vyuo Vikuu sambamba na wadau mbalimbali wa masuala ya uwezeshaji wanawake kiuchumi na Vijana.
Mhe. Mahawanga amewataka Mabinti na Vijana wote wenye vipaji na mawazo ya maendelo katika Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwani Taasisi ya Tisha Mama Foundation itawasaidia kugeuza Vipaji na Mawazo yao kuwa fursa lakini pia amewaahidi kuwa nao bega bega kuwasaidia mpaka kufikia lengo kubwa la kuhakikisha vijana na Wanawake wanajikomboa kiuchumi kupitia fursa zinazopatikana ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Aidha Mhe. Mahawanga ameeleza namna ambavyo Taasisi ya Tisha Mama Foundation ilivyoona kipaji cha pekee cha Uchoraji cha Binti Mhellepu Shillingi na kumpa Tuzo ambapo sasa amekuwa Mwalimu na sehemu ya Mabinti wengine ambao wameanza kupatiwa mafunzo ya uchoraji na kufikia katika hatua nzuri mpaka kufika mwakani 2024 mwezi wa nne watakuwa wamehitimu nao watakwenda kuwa chachu ya kuwasaidia Mabinti wenzao na vijana kiujumla.
Mhe. Mahawanga amepongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo amekuwa akiwezesha makundi mbalimbali ya Vijana na Wanawake kiuchumi na kuahidi hatokuwa nyuma katika hilo kwa kumuunga mkono Rais Dkt Samia kupitia Taasisi yake na Ofisi ya Mbunge kutoa fursa hizo kwani umekuwa ni mchango mkubwa kwa kuhakikisha kituo hicho cha Mafunzo cha Mabinti na Vijana kwenye Uchoraji kinasimama imara na kinakwenda kuleta tija kubwa kwa kuibua Vipaji kwa wengine.
Aidha Meneja Miradi wa CRDB, Ndugu. Baraka Kiyalo, amepongeza jitihada za Tisha Mama Foundation katika kusaidia jamii hasa Mabinti, Vijana wa kiume na Wanawake na kusema benki hiyo ipo tayari kusaidia jamii kupitia taasisi hiyo kufanikisha ndoto zao na kuwafanya kunufaika na fursa mbalimbali zilizopo ikiwemo mikopo isiyo na riba ya Imbeju.
Nao Madiwani wa Viti Maalumu wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, wameipongeza Tisha Mama Foundation hususan Mbunge Mahawnga kwa jitihada kubwa zinazofanyika kuwasogeza karibu na fursa na kuwataka wasichana hao walioanza kupata mafunzo hayo kueneza fursa hiyo kwa wenzao wengine na kuahidi kushirikiana na Mbunge Mhe. Mahawanga sambamba na Taasisi ya Tisha Mama Foundation kwenye maeneo yao kuibua vipaji mbalimbali vya Mabinti na Vijana na kuangalia namna bora ya kuwawezesha.
Pia Mkufunzi wa Uchoraji Bi. Mhellepu, ameishukuru Tisha Mama Foundation kwa kuwawezesha kimafunzo na kwamba dhamira yao ni kuwa wachoraji wakubwa wa Kimataifa na kutumia vipaji vyao kuwa fursa ya ajira ambapo pia Mkuu wa Don Bosco Upanga, Father Peter Mkechura, alisema kituo hicho kinaishukuru Tisha Mama Foundation kwa kuwa mdau muhimu kusaidia Mabinti hao kutimiza ndoto zao na kuomba jamii kusaidia watoto wenye Vipaji kuonyesha taranta walizonazo.
Tags
Habari