AONDOLEWA KWENYE USIMAMIZI WA VISIMA NA MABWAWA KWA KUTOFIKA HANANG


Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) leo tarehe 08 Desemba, 2023 amefanya Mabadiliko kwa kumteua Mhandisi Ndele Mengo kuwa Mkurugenzi, Sehemu ya Uchimbaji wa Visima na Ujenzi wa Mabwawa, ambaye awali alikuwa Mkurugenzi wa Ufundi RUWASA.

Mhandisi Ndele anachukua nafasi ya Mhandisi Mashaka Sitta.
Waziri Aweso amefikia maamuzi haya baada ya Mhandisi Sitta   kutotimiza vema majukumu yake katika eneo hili muhimu la uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa na usimamizi wa mitambo na zaidi kutofika wilayani Hanang mkoani Manyara baada ya kutokea changamoto ya mafuriko yaliosababisha uharibifu wa miundombinu ya Maji.

Ameeleza kuwa mabadiliko haya yamelenga kuimarisha sehemu ya uchimbaji wa visima na ujenzi wa mabwawa na kusisitiza kuwa mchakato wa uundwaji wa Wakala kamili wa DDCA unaendelea na utakamilika kwa wakati.

Aidha Waziri Aweso amemuelekeza Mhandisi Ndele Mengo kufika mara moja Wilayani Hanang na kuanza kazi ya usimamizi wa uchimbaji wa visima kwa maeneo ambayo Miundombinu ya Maji imeathiriwa na mafuriko.

Katika hatua nyingine Waziri Aweso amemteua Mhandisi Mariam Majala kuwa Mkurugenzi Msaidizi wa Ufundi, RUWASA ambaye  alikuwa Meneja wa RUWASA mkoa wa Simiyu na 
Mwisho amemteua Mhandisi Abbas Pyarali kuwa Mkurugenzi Msaidizi, Sehemu ya Usanifu na Usimamizi wa Miradi ya Maji Wizara ya Maji, awali alikuwa Mhandisi Mkuu katika Idara ya Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira, Wizara ya Maji.

Waziri Aweso amefanya uteuzi huu kwa mamlaka aliyonayo kupitia Sheria Namba 5 ya Mwaka 2019 ya Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira.

Post a Comment

Previous Post Next Post