Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Jasmine Kairuki, (Mb), leo tarehe 18 Oktoba, 2023 kwa mara ya kwanza ameshiriki Mkutano Mkuu wa 25 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), unaoendelea Jijini Samarkand, Uzbekistani akiwa Makamu wa Rais wa Shirika hilo ngazi ya dunia.
Hatua hiyo imefuatia kuthibitishwa kwa Tanzania na Nchi Wanachama wa Umoja huo duniani kuwa Makamu wa Rais wa Rais wa Shirika hilo.
Mhe. Kairuki amezishukuru nchi wanachama wa UNWTO kwa kuichagua nchi ya Tanzania katika nafasi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa karibu na nchi hizo ili kukuza na kuendeleza Sekta ya utalii duniani.
Tanzania pamoja na Moroko zilishinda nafasi hiyo kuliwakilisha Bara la Afrika katika uchaguzi uliofanyika Mauritius Julai mwaka huu nchini Mauritus wakati wa Mkutano wa Kanda ya Afrika na katika Mkutano huo wa duniani zilihitajika kura za wanachama kutoka mabara mengine ili kuthibitishwa katika nafasi hizo.
Mkutano huo unaoendelea nchini Uzbekistani ulifunguliwa tarehe 16 Oktoba, 2023 na Rais wa Uzbekistan, Mheshimiwa Shavkat Mirziyoyev na unahudhuriwa na Mawaziri wa Utalii kutoka Nchi wanachama wa UNWTO zaidi ya 121 pamoja na Mashirika ya Kimataifa, Taasisi za kifedha na wadau kutoka sekta binafsi.
