Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam Mh. Mahawanga Janeth ametunukiwa Tuzo kama Kiongozi Kinara katika Ustawi wa Mabinti na Vijana.
Mh. Mahawanga katika utendaji majukumu yake amekuwa mama na dada imara ambaye yupo karibu sana na Mabinti na Vijana wa ndani na nje ya Mkoa wa Dar es Salaam. Kupitia kitengo cha Mabinti cha Tisha Dadaz ndani ya Taasisi yake ya Tisha Mama Foundation ambayo inaunganisha Mabinti katika kuinua na kuendeleza vipaji vyao, kusimamia shughuli zao na kubwa zaidi kuhakikisha kila binti mwenye nia ya maendeleo na mchapa kazi haachwi nyuma.
Lakini kubwa zaidi ni nia yake ya kuhakikisha kila Binti na Kijana anatimiza ndoto zake. Amekuwa akiwatia moyo na kuwaunganisha Mabinti na Vijana wa vyuo, Wajasiriamali, Wabunifu na ambao wanatamani kutimiza ndoto zao lakini hawaoni pa kuanzia. Hili limefanikiwa sana baada ya kuwaunganisha Vijana waliokwisha fanikiwa na wale wenye ndoto zinazofanana nao ili kuwashika mkono na kuwaonyesha njia sahihi na Wadau sahihi wa kuwafikisha kilele cha kutimiza ndoto zao.
Mh. Mahawanga ameipongeza sana Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye Taifa letu lakini pia kwa kuona umuhimu wa uwezeshwaji kwa Vijana kupitia mikopo ya Halmashauri, vilevile kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana, Ajira na wenye Ulemavu kuwa na mikopo kwa ajili ya vijana.
Mh. Mahawanga amefanikiwa sana katika kuwaunga Vijana kuhakikisha waliomaliza vyuo ambao wanauelewa mpana wa kuandaa maandiko ya miradi na wana jicho kubwa kwenye kuziangalia fursa kwa kuwaunga na wenzao ambao hawakufika vyuoni ila wameshaanza shughuli za ujasiriamali ili kwa kutumia uzoefu wao waungane kwenye vikundi ili kupata mitaji na kufanya kazi kwa pamoja na kuwekeza kwenye miradi yenye tija na kutengeneza ajira miongoni mwao.
Mh. Mahawanga pia amekuwa akiwasihi sana Mabinti na Vijana kuhakikisha wanasimamia ndoto zao na kujitambua wanataka nini au wanataka kuwa akina nani. Lakini kwenye safari yao wasisahau kuziishi J kumi ambazo ni Jitambue, Jiamini, Jibrand, Jikubali, Jifunze sana, Jisimamie mwenyewe, Jichanganye na wengine, Jitoe kwa ajili ya wengine, Jitenge na fikra potofu zitakazikurudisha nyuma na Jitume sana.
Mh. Mahawanga amekuwa akiwasihi sana akina mama kuhakikisha wanapata muda wa akuongea na Vijana majumbani lakini pia kuwashirikisha kwenye shughuli zao mbalimbali ili kuwapa uzoefu kwani sasa ni wakati wa kuwaandaa akina mama na akina baba bora wa kesho.
