WAZIRI MAVUNDE ATOA MAAGIZO MAZITO KWA WATENDAJI JUU YA UKUSANYAJI WA MADUHULI KUPITIA SEKTA YA MADINI

 


Waziri wa Madini Mh. Anthony Mavunde amewataka watendaji wote wa wizara ya madini kuhakikisha wanasimamia ukusanyaji maduhuli kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili kufikia lengo la makusanyo ya Shilingi Trilioni moja kwa mwaka 2023/24.

Hayo yamesemwa jana tarehe 14 Septemba, 2023 na Waziri wa Madini, Mh. Anthony Mavunde alipokutana na watumishi wote wa Wizara ya Madini kwa lengo la kuweka mikakati bayana ya utekelezaji wa vipaumbele vya Wizara.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mh. Dkt.Samia Suluhu Hassan , Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa maduhuli kufikia shilingi trilioni moja kwa mwaka 2023/24. 

Kipimo chetu katika Wizara hii ni kufikia lengo la kukusanya maduhuli shilingi trilioni moja kwa mwaka 2023/24 kutoka zaidi ya shilingi bilioni 648 zilizokusanywa mwaka 2022/23. 

Lazima tufanye kazi kwa ushirikiano, bidii, uaminifu na weledi wa juu ili kufikia lengo hili,sitosita kuchukua hatua kwa wale wote ambao watakuwa kikwako katika kufanikisha ukusanyaji wa mapato kupitia sekta ya madini.

Lakini pia hatua stahiki na kali zitachukuliwa kwa watoroshaji wote wa madini ambao wanaikosesha mapato nchi yetu ya Tanzania.

Wizara imekuja na muelekeo mpya ujulikanao kama "Vision 2030 - Madini ni Maisha na Utajiri" mpango ambao umelenga kuongeza mchango wa upatikanaji wa rasilimali fedha kwa Serikali na kuinua maisha ya wananchi kwa ujumla kupitia sekta ya madini.

Utajiri wa sekta hii ni taarifa sahihi za uwepo wa madini kwenye miamba, ndiyo maana kupitia Vision 2030 tunakwenda kuhakikisha tunatumia teknolojia ya kisasa ya ' _High Resolution Airborne Geophysical Survey_ ' kupiga picha eneo lote la Nchi yetu ili kuwa na taarifa za kiasi cha madini kinachopatikana kila eneo"Alisema Mavunde

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Ndugu Kheri Mahimbali ameahidi kumpa ushirikiano Mhe. Waziri Mavunde na kusisitiza atasimamia maelekezo yote yatolewao katika kufanikisha Vision 2030 kwa ustawi wa sekta, wananchi na uchumi wa Nchi yetu.


Naye Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Lemomo Kiruswa alimpongeza Mhe. Mavunde kwa kuja na muelekeo mpya katika sekta ya madini kufikia mwaka 2030. Aidha, Mhe. Kiruswa alieleza kuwa kazi pekee iliyobaki ni kwa wataalam kuyabeba maono hayo na kuyatengenezea mpango wa utekelezaji (Road map toward Vision 2030) ambao utakuwa unapimika katika kipindi cha Mwezi, Robo mwaka au Mwaka ili kutathmini hatua tunayokuwa tumeifikia.

Post a Comment

Previous Post Next Post