SERIKALI KUWEKA TAA KWENYE BARABARA ZOTE KATIKA MIJI: BASHUNGWA



Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imesema itahakikisha inatenga bajeti ya kutosha ya kuweka taa katika barabara zote zinazopita katika miji ili wananchi waweze kufurahia matunda ya uwepo wa barabara hizo na kusaidia katika masuala ya ulinzi.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Ujenzi Mhe. Innocent Bashungwa, mbele ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Sabasaba, Newala  mkoani Mtwara ikiwa ni muendelezo wa ziara ya Mhe. Rais katika mikoa ya Kusini.


Aidha, Waziri Bashungwa amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wanaondelea kutekeleza mradi wa barabara kuanzia Mnivata hadi Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami ili kazi iweze kukamilika kwa viwango vya juu.


“Niwaombe wananchi wa Mtwara mtoe ushirikiano kwa wakandarasi na muwe sehemu ya miradi hii, kwa upendo wake alionao kwa wananchi wa hapa, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta mabilioni ili tuweze kujenga lami kwa viwango vya juu”, amesisitiza Bashungwa.

Post a Comment

Previous Post Next Post