Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Mh. Anthony Mavunde ameahidi kuvizewesha vikundi vya wananchi wa Dodoma kupata mashine za utengeneza mkaa kwa kutumia makaratasi na taka ili kuunga mkono jitihada za kutunza mazingira kwa kutumia nishati safi ambayo ambayo haina athari kwa mazingira.
Mavunde ameyasema hayo leo katika Viwanja vya Nyerere Square Dodoma wakati wa hafla fupi ya kugawa majiko ya gesi kwa Mama Lishe 205 wa kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma.
“Ni mpango wa serikali chini ya uongozi wa Mh Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwawezesha wakina mama kiuchumi ili waweze kuimarika.
Matumaini yangu kwamba majiko haya yatasaidia kuchochea shughuli zenu za kiuchumi na kuongeza ufanisi katika huduma za lishe mnazotoa ikienda sambamba na utunzaji wa mazingira.
Nimefanya mazungumzo na TEMDO. kupata mashine ndogo ambazo zitasaidia sana wananchi kutengeneza mkaa ambao hautokani na kukata miti ili wale wanaotegemea uuzaji mkaa kuendesha maisha yao waendelee kufanya biashara hiyo lakini kwa kuzalisha mkaa ambao unatengenezwa kupitia makaratasi na taka pasipo kukata miti na kuathiri mazingira”Alisema Mavunde
Akishukuru kwa niaba ya Mama Lishe wote,Diwani wa Kata ya Chinga Mh.Allice Kitendya amemshukuru Mbunge Mavunde kwa mara zote kuwakimbilia na kuwawezesha wakina mama na kuahidi kwamba majiko hayo yatakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi ya wakina Mama.
