WAZIRI UMMY AFUNGA KONGAMANO LA KUWAWEZESHA WANAWAKE KIUCHUMI



Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu tarehe 24/08/2023 amefunga kongamano la kuwawezesha wanawake kiuchumi lililoandaliwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga Mhe. Eng. Mwanaisha Ulenge.


Akifunga Kongamano hili, Mhe Ummy alimpongeza Mhe Eng Mwanaisha Ulenge kwa kuandaa Kongamano zuri lililoleta watoa mada mahiri kutoka Taasisi mbalimbali nchini na hivyo anaamini limenufaisha wanawake wengi kupata Elimu, Taarifa na Maarifa kuhusu masuala mbali yanayohusu fursa za kibiashara.


Aidha Mhe Ummy amewataka wanawake wajasiamali waliopata Elimu katika kongamano hilo kujiunga katika vikundi vya wajasiriamali hususani kupitia Majukwaa ya Uwezeshaji wanawake kiuchumi yaliyokatika ngazi ya Mitaa, Kata na Halmashauri ili kufikiwa kwa urahisi sambamba na kupata fursa mbalimbali za kujiendeleza kiuchumi.

Aidha Mhe Ummy amewataka wanawake hao pia kuchukua hatua za kujilinda na kujikinga na magonjwa yasiyo ya kuambukiza hususani Kisukari, Shinikizo la juu la damu na Saratani kwa kupima afya zao angalau mara moja kwa mwaka kwa kueleza kuwa afya njema ni msingi wa uchumi imara wa mtu mmoja mmoja, jamii na Taifa kwa ujumla.


Nae Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tanga Mhe Eng. Mwanaisha Ulenge alieleza kuwa ameandaa kongomano hilo ikiwa ni kutambua wajibu alio nao katika kuwaunganisha wanawake wa wilaya zote za Mkoa wa Tanga ili kujikomboa kiuchumi ndio maana ameliita Kongamano hili kama "Daraja" la kuwaunganisha na kuwavusha wanawake kutoka hatua moja hadi nyingine kiuchumi. 


Kongamano hilo la siku mbili lilifunguliwa na Mhe Dkt Dorothy Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kasimu Majaliwa Majaliwa chini ya Kauli mbili ya Wanawake na Fursa za Kibiashara kupitia Bomba la Mafuta..

Post a Comment

Previous Post Next Post