MPANGO WA UWEKEZAJI AFYA YA MAMA NA MTOTO WAZINDULIWA ZANZIBAR



Makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mhe. Othman Masoud Othman amezindua Mpango wa Uwekezaji wa Afya ya Mama na Mtoto Tanzania wa miaka mitano (Tanzania Martenal & Child Health Investment Program) wenye lengo la kuimarisha afya ya Mama na mtoto nchini unaofadhiliwa na Benki ya Dunia pamoja na Shirika la Global Financing Facility. 


Akizundua Mpango huo leo Agosti 23,2022 Zanzibar .Mhe Othman amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe  Dkt. Samia Suluhu Hassan  na Rais wa  Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi  Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi  kwa kuendelea kutoa kipaombele katika sekta ya afya  na  kuwezesha uzinduzi wa mpango  wa uwekezaji  katika afya ya mama na mtoto unaolenga kuboresha huduma ya afya ya mama na mtoto katika ngazi zote Tanzania Bara na Zanzibar.


Amesema Mpango huo utatekelezwa chini ya usimamizi wa Wizara ya Afya Tanzania Bara,  Wizara ya Afya Zanzibar pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambapo uwekezaji wake utagharimu dola za Marekani milioni  275 na kati ya hizo dola za Marekani 250 ni mkopo wa gharama nafuu kutoka Benki ya Dunia na  dola za Marekani milioni 25  kutoka Global financing facility.


Mhe. Othman amesema  kuwa, kwa upande wa Tanzania Bara Mpango huu utatekeleza afua muhimu ikiwemo kuajiri watumishi 1, 000 wa kada mbalimbali za afya, kufanya ukarabati wa vituo 159 vya kutolea huduma za afya na ununuzi wa vifaa tiba kwa ajili ya utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto. 

Sanjari na hilo Mhe. Othman amesema mpango utaimarisha mfumo wa magonjwa ya dharura na rufaa kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga pamoja na kuimarisha menejimenti na uwajibikaji katika utoaji wa huduma za afya na  kwa upande wa Zanzibar mpango utaimarisha utoaji wa huduma za afya ya mama na mtoto pamoja na  kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma bora za afya kwa wananchi. 


Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Festo Dugange amesema Ofisi ya Rais-TAMISEMI  itasimamia na kufuatilia utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji wa Afya ya Mama na Mtoto (Tanzania Maternal & Child Health Investment Program)  kwenye Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa  ili kufikia  malengo yaliyokusudiwa  na Serikali.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Afya Tanzania Bara Mhe. Godwin Mollel amesema Serikali itasimamia kikamilifu fedha zitakazotolewa ili kufikia lengo la kuboresha huduma za afya kwa jamii.

Post a Comment

Previous Post Next Post