Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki amesema mafunzo ya uongozi kwa ajili ya Wakurugenzi wote wa Mamlaka za Serikali za Mitaa yatafanyika Septemba,2023.
Mhe. Kairuki ameyasema hayo Agosti 22, 2023 alipokuwa akitoa maelezo mafupi kwenye ufunguzi wa mafunzo ya uongozi kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala Mikoa yaliyofanyika kwenye shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Amesema mafunzo hayo yalianza kwa maafisa Tarafa na Watendaji wa Kata kwenye mikoa ya Songwe, Njombe, Katavi na Rukwa kwa kwa awamu ya kwanza na yataendelea kutolewa kwa Maafisa Tarafa wa nchi nzima.
“Kwasasa tumewafikia viongozi hawa wakuu wa Mikoa na watakaofuata ni Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa,”amesema.
Waziri Kairuki amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea viongozi uwezo wa kuongoza, kuwa na maamuzi ya kimkakati na kusimamia watu, fedha na rasilimali nyingine kwa ufanisi.
Mafunzo hayo yamefunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango na mada 20 zitawasilishwa kutoka kwa watoa mada wabobezi na wenye uzoefu wa serikalini na sekta binafsi ambapo zitajikita katika masuala ya uongozi na usimamizi wa rasilimali zilizopo kwenye maeneo yao.