Waandishi nguli wa habari za michezo na burudani kutoka sehemu mbalimbali duniani walioko nchini kwa ziara ya kiutalii na kuangalia maandalizi ya Afcon 2027 jana walijionea miundombinu ya kisasa jijini Dar es Salaam ikiwemo uwanja wa Benjamin Mkapa na Gymkhana ambavyo Serikali ya Dkt. @samia_suluhu_hassan inaendelea kuvikamilisha.
Wakizungumza katika kipindi maalum walichokuwa wakirekodi jana jioni wanahabari hao na watu wenye ushawishi mitandaoni (influencers) kutoka vyombo vikubwa kama Sporty TV ya Hispania, TRT ya Canada, NWE Media ya Marekani na mainfluencer kutoka Uingereza na Ufaransa wamesema ukija Tanzania ni zaidi ya Afcon.
Wakiwa Coco Beach jana jioni walionesha kushangazwa na mandhari ya jiografia ya Tanzania hasa fukwe na vyakula vya asili.
“Hii nchi ni zaidi ya michezo. Hakika Tanzania ni nchi ya kuvutia ambayo mashabiki wakija Afcon hapa ni zaidi ya kwenda uwanjani maana kuna vivutio vingi, nina shauku kubwa ya kuionesha dunia mambo mazuri sana kutokea hapa,” anasema Haneefa Lee almaarufu @lfc_girl7 bloga, mchambuzi wa mitandanoni na shabiki mashuhuri wa klabu ya Liverpool ya Uingereza.
