Waziri wa Nishati, Dkt. Juma Homera, amesema uwezo wa uzalishaji wa umeme nchini umeongezeka na kufikia Megawati 4,646 kutoka vyanzo mbalimbali vya nishati, huku Serikali ikilenga kuongeza uwezo huo hadi Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.
Dkt. Homera amesema vyanzo hivyo ni pamoja na maji, gesi asilia, nishati ya jua na vyanzo vingine mbadala, hatua inayolenga kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya matumizi ya wananchi na shughuli za kiuchumi.
Akizungumzia hatua zinazochukuliwa kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia nishati jadidifu, amesema Serikali imekamilisha Mradi wa Kishapu I wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 50 za umeme wa jua, huku ujenzi wa Mradi wa Kishapu II wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 100 ukiendelea.
Ameongeza kuwa miradi mingine ya uzalishaji wa umeme yenye uwezo wa zaidi ya Megawati 600 ipo katika hatua mbalimbali za majadiliano na upembuzi, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.
Kuhusu miundombinu ya usafirishaji wa umeme, Dkt. Homera amesema Serikali imekamilisha Mradi wa Chalinze–Dodoma tangu Septemba 2026, ambao umeimarisha ubora na kiwango cha umeme unaofika katika mikoa ya Magharibi na Kaskazini mwa nchi.
Aidha, amesema Mradi wa Iringa–Tunduma–Sumbawanga unatarajiwa kuwashwa Novemba 2026, hatua itakayoiunganisha Rukwa katika Gridi ya Taifa kwa mara ya kwanza na kuimarisha upatikanaji wa umeme katika mkoa huo.
Amesema pia Mradi wa Chalinze–Kinyerezi–Mkuranga unatarajiwa kuwashwa Februari 2027 kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa umeme jijini Dar es Salaam na katika maeneo ya viwanda ya Mkuranga, yanayochangia ukuaji wa shughuli za kiuchumi na uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Homera amesema utekelezaji wa Mradi wa Songea–Tunduru–Masasi–Maumbika unaendelea kwa kasi, ukiwa na lengo la kuunganisha mikoa ya Lindi na Mtwara katika Gridi ya Taifa na kupunguza changamoto za upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.
Amesisitiza kuwa hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kupanua uwezo wa uzalishaji na usafirishaji wa umeme nchini, kuongeza uhakika wa huduma hiyo na kuweka mazingira bora ya kukuza uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi.
