Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, kuhusu maeneo mbalimbali ya ushirikiano na uwekezaji katika sekta ya nishati, hususan umeme, nishati jadidifu, mafuta na gesi asilia pamoja na nishati safi ya kupikia.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo, Oktoba 22, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam, Dkt. Homera amesema Tanzania inahitaji wawekezaji katika utafutaji, uzalishaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, ikiwemo ujenzi wa vituo vya kujazia gesi asilia iliyoshindiliwa kwenye vyombo vya usafiri (CNG).
Aidha, amesema Tanzania inahitaji ushirikiano wa kitaalamu na kiteknolojia katika ujenzi, uendeshaji na usimamizi wa viwanda vya kusafisha mafuta hususan wakati huu ambapo nchi ipo katika mchakato wa kuanzisha kiwanda cha kusafisha mafuta mkoani Tanga.
"Katika shughuli za utafutaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia, tunahitaji ushirikiano katika uendelezaji wa vitalu mbalimbali, ikiwemo Eyasi-Wembere na Mnazi Bay," amesema Dkt. Homera.
Kuhusu sekta ya umeme na nishati jadidifu, Dkt. Homera amesema Tanzania inahitaji uwekezaji katika miradi mbalimbali ya uzalishaji wa umeme, ikiwemo miradi ya Rumakali (MW 222), Ruhudji (MW 358), miradi ya umeme wa jua ya Zuzu, Kititimo na Same pamoja na miradi ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia upepo.
Katika eneo la nishati safi ya kupikia, amesema Kampuni za China zinazotengeneza vifaa vya kupikia zinaweza kuanzisha viwanda vya kuunganisha majiko ya umeme yenye ufanisi na majiko janja ya umeme (induction), hatua itakayosaidia kupunguza gharama za vifaa hivyo na kuwezesha kaya nyingi zaidi nchini kumudu matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema uwekezaji unahitajika pia katika uzalishaji wa nishati mbadala zilizo rafiki kwa mazingira pamoja na kuimarisha upatikanaji na usambazaji wa vifaa vya nishati safi ya kupikia.
Vilevile, Dkt. Homera amesema maeneo mengine ya ushirikiano ni pamoja na uendelezaji wa teknolojia ya nishati ya nyuklia ambayo ni rafiki kwa mazingira, upatikanaji wa mitambo na vifaa vya kisasa vya uzalishaji na usafirishaji wa umeme, pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu kupitia mafunzo, uhamishaji wa teknolojia na ubunifu.
Kwa upande wake, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema Tanzania na China zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu unaoendelea kuimarika, ikiwemo katika sekta ya nishati ambapo China imeshiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali, hususan ya usafirishaji wa umeme.
Amesema China ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya sekta ya nishati pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa ndani kupitia mafunzo na kubadilishana uzoefu.
Balozi huyo ameongeza kuwa katika mwaka 2025, China ilitoa takribani nafasi 2,000 za mafunzo kwa Watanzania katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano na kujenga uwezo wa wataalamu nchini.
