Wananchi wa Nyaruyoba na maeneo jirani sasa watapata huduma za usafirishaji wa wagonjwa wanaohitaji huduma za dharura na rufaa kwa urahisi zaidi baada ya Kituo cha Afya Nyaruyoba kupatiwa gari la wagonjwa (ambulance).
Ambulance hiyo imekabidhiwa leo, Septemba 17, 2026, na Naibu Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Muhambwe, Dkt. Florence Samizi, katika Kituo cha Afya Nyaruyoba, Kata ya Nyaruyoba, Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Mkoa wa Kigoma.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Dkt. Samizi ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo kutenga fedha za mafuta kwa ajili ya ambulance hiyo ili iwe tayari muda wote na iweze kuwafikisha wagonjwa wanaohitaji huduma za rufaa katika vituo vyenye huduma za juu bila kuchelewa.
Amesisitiza kuwa wagonjwa wanaohitaji huduma ya ambulance hiyo hawapaswi kutozwa gharama za mafuta, huku akiwataka viongozi na watumishi wa afya kuhakikisha gari hilo linatumika kwa wagonjwa wenye uhitaji na kwa madhumuni yaliyokusudiwa.
Dkt. Samizi amesema uwepo wa ambulance hiyo utaongeza uwezo wa Kituo cha Afya Nyaruyoba kutoa huduma za rufaa, hususan kwa wagonjwa wanaohitaji matibabu au huduma ambazo hazipatikani katika kituo hicho.
Amesema Serikali inaendelea kuwekeza katika sekta ya afya kwa kuboresha miundombinu, vifaa na mazingira ya utoaji wa huduma, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa wakati na karibu na maeneo wanayoishi.
Aidha, Dkt. Samizi ameitaka Halmashauri na watumishi wa afya kulitunza gari hilo, kuhakikisha linafanyiwa matengenezo kwa wakati na linakuwa tayari wakati wote wa dharura, ili liendelee kuwa msaada muhimu kwa wananchi wa Nyaruyoba na maeneo yanayozunguka kituo hicho.
