MARY CHATANDA: RAIS SAMIA, KINARA WA USTAWI NA MAENDELEO YA MTOTO


Katika kuadhimisha Siku ya Mtoto Afrika, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mary Chatanda, Juni 18, 2026, Jijini Dodoma, amesema Rais Dk. Samia ni kinara wa ustawi na maendeleo ya mtoto kwani serikali yake imeweka mazingira mazuri yenye kuchochea maendeleo ya mtoto.

Chatanda amesema serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza kikamilifu sera ya elimu bila ada ambapo serikali inagharamia elimu kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha sita, jambo linalomtengenezea ustawi mtoto.

"Rais wetu Dk. Samia anasimamia sera ya elimu bila ada hadi kidato cha sita na hata wanafunzi wakifaulu kwenda vyuo vya kati na vikuu, serikali inatoa mikopo, jambo linalomhakikishia mtoto wa Kitanzania uhakika wa kupata haki ya elimu," amesema Chatanda.

Katika hatua nyingine, Chatanda amepongeza Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia ambayo utatuzi wa kero nyingi za kifamilia na kimirathi umewezesha watoto kuishi maisha mazuri ndani ya familia zao.

"Tumeshuhudia utatuzi wa kero za ndoa, familia na mirathi kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia nchi nzima, jambo ambalo limerejesha tabasamu kwa watoto ambao walikuwa katika hatari za kuishi mazingira magumu," amesisitiza Chatanda.

Vilevile, Chatanda amesema Rais Dk. Samia amefanya kazi kubwa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi, jambo linalostawisha familia ambapo mtoto ni miongoni mwa wanufaika.

"Serikali inatoa mikopo na fursa za kuwainua kiuchumi wananchi ambapo watoto ni miongoni mwa wanufaika kupitia wazazi, walezi na ndugu zao kwani wanawezesha kuwapatia watoto wao mahitaji muhimu," amesema.

Sanjari na hilo, Chatanda amesisitiza Rais Dk. Samia ni kiongozi mwenye upendo na huruma kwa watoto na wananchi ndiyo maana mwezi Machi mwaka huu, aliamua kumuasili mtoto aliyetelekezwa wilayani Nzega mkoani Tabora. Baada ya kumuasili mtoto huyo, kwa heshima yake, mtoto huyo akapewa jina la Grace Samia Suluhu Hassan.

"Rais wetu aliamua kumuasili mtoto aliyetelekezwa kule Nzega na kuamua kuishi nae Ikulu na kuahidi kumpa malezi, ulinzi na huduma zote muhimu, huu ni upendo wa aina yake, na inathibitisha kuwa anajali maendeleo ya mtoto," amesema.

Wadau mbalimbali wamehimiza malezi bora kwa watoto ili kuwajenga katika maadili na tabia njema kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Post a Comment

Previous Post Next Post