Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo Januari 4, 2025 amezindua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi mkubwa wa maji uliopo katika kata ya Arri, Halmashauri ya Wilaya ya Babati Vijijini mkoani Manyara unaotajwa kugharimu Shilingi bilioni 2.6.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo Prof. Kitila amesema moja ya azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni 'kumtua mama ndoo kichwani' hivyo ni furaha kubwa kuona mradi huo umekamilika na kwamba unaenda kuwahudumia wakazi wa kata ya Arri, wa vijiji zaidi ya saba.
Sambamba na hilo Prof. Kitila amewasifu na kuwashukuru wadau wa maendeleo ambao ni Shirika la Karimu kwa kusaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha kukamilika kwa skimu hiyo ya maji kwa kuchangia zaidi ya bilioni 2 hivyo kuharakisha kukamilika kwa mradi huo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini Daniel Sillo amewashukuru wananchi kwa kujitolea kuchimba mitaro, kulaza mabomba na kufukia mitaro ya maji, hatua ambayo imetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa mradi huo ambao unakwenda kumaliza tatizo la maji lililodumu kwa muda mrefu kwenye zaidi ya vijiji sita ambavyo ni Managha, Dudiye,Dohom, Endasago, Arri, Sharmo na Tsaayo.