UTOAJI WA TAARIFA KWA WANANCHI UWE ENDELEVU


Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Festo Dugange amewataka Wakuu wa Mikoa na  Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa  kuhakikisha utoaji wa  taarifa za utekelezaji wa miradi kwa wananchi unakuwa endelevu na si kusubiri kampeni au tukio maalum.

Dkt. Dugange ametoa wito huo leo Novemba 1,2023 wakati akizindua Kampeni  ya Tumewasikia, iliyoandaliwa  na Idara ya Habari Maelezo.
‘Wizara inawasisitiza Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha utoaji wa taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo unakuwa endelevu,’ amesisitiza Dkt. Dugange

Amesema Serikali inataka kuona Wakuu wa Mikoa, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara na wataalam wote wa Serikali wanatoa taarifa kwa wakati ili wananchi wajue hatua zilizochukuliwa na Serikali kuwaboreshea huduma.

Ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa,Dkt. Dugange amewataka watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoa ushirikiano kwa msemaji Mkuu wa Serikali kila atakapohitaji taarifa za kuuhabarisha umma. 

Dkt. Dugange amewataka viongozi hao kuwashirikisha katika matukio na kuwapa ushirikiano maafisa habari waliopo katika maeneo yao ili waweze kutekeleza  jukumu la kuuhabarisha umma kwa ufanisi. 

Ili kuboresha utendaji kazi, Dkt. Dugange amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri ambao hawana maafisa habari kuhakikisha wanaaajiri maafisa hao kwa  mikataba  wakati wanasubiri Serikali ikamilishe taratibu za kuwaajiri.

Post a Comment

Previous Post Next Post